Na
Zuena Msuya Dodoma,
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard
Kalemani amelitaka na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)
kuharakisha uunganishaji wa huduma ya gesi asilia katika baadhi ya nyumba za
wananchi kwenye maeneo ya jiji la Dar Es Salaam kwa ajili ya matumizi ya
nyumbani.
Dkt.Kalemani aliyasema hayo
ofisini kwake mkoani Dodoma alipokutana na watendaji wa TPDC kwa lengo la
kujadili suala la usambazaji wa Gesi asilia katika nyumba za Wananchi pamoja na
bei watakayouziwa wananchi hao.
Katika mazungumzo hayo, Dkt.
Kalemani aliwataka TPDC kuunganisha nyumba
kuanzia Hamsini( 50) na kuendelea, na
huduma ya gesi asilia katika maeneo la
Mwenge na Mikocheni, kwa kuwa tayari miundombinu ya bomba la gesi asilia kwa
matumizi ya nyumbani imepita maeneo hayo.
Wakizungumzia suala la bei ya
kuwauzia wateja, Dkt. Kalemani alisema kuwa pamoja na mambo mengine Gesi hiyo
itauzwa kwa Wananchi kwa pungufu ya 40% ya bei ya mitungi ya gesi itayokuwa
sokoni kwa wakati huo.
" Hii ni gesi yetu na bomba
ni la kwetu vyote vinapatikana hapahapa nchini, ni vyema iuzwe kwa bei ya chini
zaidi ya ile iliyopo sokoni kwa sasa, ili kila mwananchi aweze kumudu gharama
zake pia ni rafiki wa mazingira, itasaidia kupunguza matumizi ya mkaa na
kulinda misitu yetu", alisema Dkt. Kalemani.
Hata Hivyo Dkt. Kalemani
aliwaagiza TPDC kuendelea na taratibu za kuwaunganisha wananchi wa Mtwara na
huduma ya gesi asilia katika nyumba zao kwa matumizi ya nyumbani kama
itavyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.
Aidha amelishauri shirika hilo,
kutumia wataalamu wake wa ndani kupitia shirika lake la kulinda miundombinu ya
gesi (GASCO) ili kusambaza gesi asilia kwenye nyumba za wananchi kwa ajili ya
matumizi ya nyumbani badala ya kutegemea wakandarasi ambao mchakato wa kuwapata
unachukuwa muda mrefu.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi
wa TPDC, Mhandisi Kapuulya Musomba, alifafanua kuwa gharama za uunganishwaji wa
huduma ya gesi asilia katika nyumba za wananchi itategemea na ramani ya nyumba
husika pamoja na umbali wa nyumba hiyo kutoka ilipopita miundombinu ya bomba la
gesi asilia linalotumika kusambaza gesi katika maeneo ya makazi.
Vilevile, Mhandisi Musomba
aliweka wazi kuwa mfumo wa kusambaza gesi asilia katika nyumba za wananchi utakuwa
kama ule unaotumika kusambaza huduma ya maji, lakini ulipaji wa gharama za
matumizi ya gesi hiyo utakuwa kama ule unaotumiwa na Shirika la Umeme Tanzania
(TANESCO), Lipa Umeme Kadri Unavyotumia (LUKU) kwa maana kwamba kila mtumiaji
wa gesi asilia nyumbani kwake atalipia huduma hiyo kwa kadri atakavyokuwa
akitumia.
Gesi itakayokuwa ikisambazwa kwa
ajili ya matumizi ya nyumbani ni ile inayozalishwa katika Visima vya gesi
vilivyopo katika Mkoa wa Lindi na Mtwara.
|
Waziri wa Nishati, Dkt Medard
Kalemani akizungumza na watendaji wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania
(TPDC) na watendaji wa Wizara ya Nishati, kuhusua suala la usambazaji wa gesi
asilia katika nyumba za wananchi kwa ajili ya matumizi ya nyumbani, ofisini
kwake mkoani Dodoma
|
|
Waziri
wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (kushoto) na Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la
Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Mhandisi Kapuulya Msomba (kulia) wakizungumza
kuhus suala la usambazaji wa gesi asilia katika nyumba za wananchi kwa ajili ya
matumizi ya nyumbani.
|