Saturday 14 April 2018

Kampuni kutoka China yaomba kuwekeza Sekta ya Nishati


  • Waziri Kalemani asema wanakaribishwa ikiwa wana vigezo
Na Veronica Simba – Dodoma
Wawekezaji kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd ya China wamemtembelea Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani na kumweleza nia yao ya kuwekeza katika sekta ya nishati nchini; hususan kwenye sekta ndogo ya gesi asilia.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia), akiwa na baadhi ya wajumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China (kushoto), baada ya kuzungumza nao kuhusu nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini. Ujumbe huo ulimtemtembelea Waziri Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma Aprili 11, 2018.

Ujumbe huo kutoka China ukiongozwa na Mwenyekiti wa Kampuni hiyo, Li Zemng, waliwasilisha maombi husika kwa Waziri na timu yake ya wataalam kutoka wizarani na TANESCO, Aprili 11, 2018 Makao Makuu ya Wizara mjini Dodoma.

Zemng alimweleza Waziri Kalemani kuwa nia yao ni kuwezesha usafirishaji wa gesi asilia katika maeneo mbalimbali nchini ambako bomba la gesi halifiki kwa kutumia teknolojia maalum.

“Tutatumia teknolojia maalum kuigeuza gesi asilia katika hali ya kimiminika (Liquefied Natural Gas – LNG), kisha tutaihifadhi katika makontena maalum na kuyasafirisha kwenda maeneo mbalimbali ambako itatumika kwa shughuli mbalimbali za maendeleo,” alifafanua Zemng.

Akijibu maombi hayo, Waziri Kalemani alisema Serikali inakaribisha wawekezaji katika sekta husika lakini akatahadharisha kuwa ni lazima wawe na vigezo stahiki.

Alitoa mwongozo kwa Kampuni hiyo kuwasilisha maombi yao rasmi kimaandishi ili yafanyiwe kazi. Aidha, aliwataka kukutana na timu ya wataalam kutoka wizarani na TANESCO ili wajadiliane kwa kina kuhusu maombi hayo ya uwekezaji ili kujiridhisha kabla ya kuwapatia jibu rasmi.

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto), akizungumza na Ujumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China (kulia), walipomtembelea na kuwasilisha nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini, Aprili 11, 2018. Wengine pichani ni wataalam kutoka wizarani na TANESCO.

Ujumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China wakiwa katika kikao baina yao na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani), walipomtembelea na kuwasilisha nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini, Aprili 11, 2018 mjini Dodoma.

Wataalam wa Wizara ya Nishati na TANESCO wakiwa katika kikao cha Waziri Dkt Medard Kalemani (hayupo pichani) na Ujumbe kutoka Kampuni ya Hainan Zhenrong Energy Ltd kutoka China (hawapo pichani), walipomtembelea na kuwasilisha nia yao ya kuwekeza kwenye sekta ya nishati nchini, Aprili 11, 2018 mjini Dodoma.