Saturday, 14 April 2018

Kumekucha Ngara….

  • Waunganishwa kwenye Gridi ya Taifa

Na Veronica Simba - Ngara

Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imeunganishwa kwenye umeme wa Gridi ya Taifa na kuachana na matumizi ya umeme wa mafuta ya dizeli.

Hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani humo ilifanyika Aprili 8 mwaka huu na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali, Vyama vya Siasa, Dini na wananchi ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.

Meneja wa TANESCO Mkoa wa Kagera, Mhandisi Francis Maze, akielezea mawanda ya Mradi huo alisema umehusisha kujenga njia ya umeme ya msongo wa kilovoti 33, yenye urefu wa kilomita 42 kutoka Nyakahura wilayani Biharamulo hadi Benaco wilayani Ngara.

Vilevile, alisema Mradi umejumuisha kazi ya kujenga njia za umeme za michepuko za msongo wa kilovoti 33 zenye jumla ya urefu wa kilomita 27.5 ili kulisha umeme katika vijiji vya Kabulwanzwiri, Kabaheshi, Lukore, Kibilizi na Keza Sekondari.

“Hii inafanya jumla ya urefu wa njia za umeme za msongo wa kilovoti 33 zinazojengwa kuwa kilomita 69.5,” alifafanua Mhandisi Maze.

Aidha, alitaja kazi nyingine kuwa ni kujenga na kuweka mashine umba (Transfoma) 10 kwa vijiji na vitongoji vilivyohusishwa na Mradi.
Nyingine ni ujenzi wa njia za msongo mdogo wa umeme zenye jumla ya kilomita 19 katika vijiji 10 vilivyonufaika na Mradi.

Kuhusu idadi ya wateja watakaonufaika na Mradi huo, Mhandisi Maze alisema kuwa jumla yao ni 482 kutoka katika vijiji vya Nyantama (53), Nyabugombe (74), Lukole (51), Kabaheshi (101) na Kabulwanzwiri (58).
Vijiji vingine ni Kumyaga (20), Mtega (68), Gwishushi (17), Kibilizi (30) na Keza (10).

Manufaa makubwa ambayo Mhandisi Maze alisema TANESCO itayapata kutokana na Mradi huo wa kuiunga Ngara kwenye umeme wa Gridi ya Taifa ni kupungua kwa gharama za uendeshaji ambapo sasa shirika hilo litapata nafuu ya asilimia 73.4 katika gharama za kupata Uniti moja ya umeme. Aidha, wananchi watapata umeme wa uhakika zaidi.

Hata hivyo, Meneja huyo wa Mkoa wa Kagera alitaja changamoto kubwa ambazo Ofisi yake inakabiliana nazo kuwa ni uchakavu wa miundombinu ya usambazaji umeme, hususan njia za umeme za Msongo wa kilovoti 33 za Muleba, Kanyigo na Karagwe.

Alitaja changamoto nyingine kuwa ni wananchi kuzuia kukatwa kwa matawi ya miti yanayosonga njia za umeme mkubwa na kuipeleka TANESCO Mahakamani pale inapolazimu kukatwa kwa miti hiyo.

Nyingine ni wananchi kupanda miti ya mbao jirani mno na njia za umeme na kusababisha miti hiyo kugusa nyaya kukiwa na upepo mkali hivyo kusababisha kukatika kwa umeme.

Changamoto nyingine iliyotajwa kuikabili TANESCO mkoani Kagera kuwa ni wananchi kuchoma nguzo za umeme, hususan za njia za umeme zilizopita mashambani.

Aliwataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Shirika hilo ili kuepusha na kutatua changamoto hizo, hali itakayosaidia kuboresha zaidi huduma zao na hivyo jamii kunufaika zaidi.


Mkuu wa Wilaya ya Ngara Luteni Kanali Michael Mtenjele (kushoto) akimkaribisha Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kushoto), alipowasili wilayani humo Aprili 8, 2018 kufungua matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa.


Sehemu ya viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa wakiwa katika hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.

Msimamizi wa Kituo cha kuzalisha umeme Ngara, Abeid Pastory (wa pili – kulia), akimweleza Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (kulia) namna Kituo hicho kinavyofanya kazi wakati wa ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani humo, Aprili 8 mwaka huu.