Na
Veronica Simba - Ngara
Serikali imelipongeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kutokana na utendaji kazi wake mzuri katika kuwapatia watanzania kote nchini huduma ya nishati ya umeme.
Waziri wa Nishati Dkt.
Medard Kalemani akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa
Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu.
|
Pongezi hizo zilitolewa
hivi karibuni, Aprili 8 mwaka huu, na Waziri wa Nishati Dkt Medard Kalemani
wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani
Ngara.
“Nalipongeza Shirika
letu la TANESCO. Kwakweli Shirika hili limebadilika sana kiutendaji, hasa
katika Menejimenti na wafanyakazi. Wanafanya kazi kwa kujituma. Baadhi ya watu
walizoea kulibeza Shirika hili lakini wanajitahidi sana kwa sasa,” alisema
Waziri.
Waziri alisema kuwa
kazi ya Serikali kupitia Wizara ya Nishati ni kulisimamia Shirika hilo ili
liendelee kufanya kazi nzuri kwa manufaa ya wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa matumizi ya umeme wa Gridi ya Taifa wilayani Ngara, Aprili 8 mwaka huu. |
Akizungumzia Mradi huo
wa kuiunganisha Ngara na umeme wa Gridi ya Taifa, Waziri Kalemani alisema kuwa
ni wa manufaa makubwa kwani utapunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uendeshaji
na hivyo kuliongezea shirika uwezo zaidi wa kuwahudumia wananchi.
“Kwa kutumia mafuta,
Uniti moja ilikuwa inawagharimu TANESCO shilingi 578 wakati huu wa Gridi
utawagharimu shilingi 154 tu kwa Uniti,” alifafanua.
Waziri aliwataka
watendaji wa TANESCO kuhakikisha wanawahudumia wana-Ngara na watanzania wote
kwa ubora zaidi kutokana na uwepo wa umeme wa Gridi ya Taifa katika maeneo
mengi zaidi na kuondokana na ule wa mafuta ambao una changamoto kadhaa.
Aidha, Dkt. Kalemani
alibainisha kuwa, sambamba na zoezi la kuhakikisha Tanzania nzima inaunganishwa
na umeme wa Gridi ya Taifa, pia Serikali inaendelea kupeleka umeme vijijini
kupitia miradi inayotekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Alisema kuwa, kufikia
mwaka 2020, hakuna kijiji kitakachobaki bila kuwa na umeme.
Aliipongeza Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais John Magufuli kwa dhamira yake ya dhati
katika kuhakikisha inawaondolea watanzania kero na changamoto mbalimbali
ikiwemo ya umeme.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Mhandisi Dkt. Tito Mwinuka pamoja na kumuunga
mkono Waziri kwa kuipongeza Serikali ya Awamu ya Tano; aliipongeza Wizara ya
Nishati inayoongozwa na Dkt Kalemani ambayo alisema ndiyo msimamizi mkubwa wa
shughuli zinazotekelezwa na shirika hilo.
Alisema kuwa, kwa
kuiunga Ngara na umeme wa Gridi ya Taifa, kiasi kikubwa cha fedha kitaokolewa.
“Kwa harakaharaka, tutaweza kuokoa takribani shilingi bilioni mbili kwa mwaka
baada ya kuzima mitambo hii ya mafuta.”
Aliongeza kusema kuwa
TANESCO itaendelea kuzima vituo vya mafuta sehemu mbalimbali nchini ambapo
itasaidia kupunguza gharama za kufua umeme kwa kutumia mafuta.
Awali, akiwasilisha
taarifa ya TANESCO kwa Mkoa wa Kagera, Meneja wake, Mhandisi Francis Maze
alisema kuwa kabla ya kuunganishwa kwenye Gridi ya Taifa, Wilaya ya Ngara
ilikuwa ikitumia umeme wa mafuta ambapo mahitaji ya juu kwa Wilaya hiyo ni
megawati 1.38.