Saturday 14 April 2018

Waziri Kalemani ajadili na AfDB kuhusu Miradi ya Nishati wanayoifadhili


Na Veronica Simba – Dodoma

Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani ameshiriki majadiliano ya maendeleo ya miradi mbalimbali ya Serikali inayofadhiliwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Majadiliano hayo yalifanyika Aprili 11 mwaka huu Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango Dodoma na kuwashirikisha Waziri husika, Dkt. Philip Mpango, Waziri Kalemani, mwakilishi kutoka Wizara ya Fedha ya Zanzibar, Halima Wagao, wataalam mbalimbali wa Wizara hizo na Ujumbe kutoka AfDB.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kalemani aliipongeza na kuishukuru Benki hiyo kwa ushirikiano ambao imekuwa ikiuonesha, hususan katika kufadhili miradi mbalimbali ya maendeleo kwa sekta ya nishati.

Miradi ya nishati iliyojadiliwa katika kikao husika ni pamoja na wa Malagarasi unaohusisha kuzalisha umeme wa megawati 45 pamoja na mradi wa kuzalisha umeme wa Kakono wenye megawati 87.

Aidha, miradi mingine ni pamoja na wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Rusumo hadi Nyakanazi na wa kusafirisha umeme wa kilovoti 400 kutoka Singida – Arusha hadi Namanga. Vilevile, mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 400 kwa umbali wa kilomita 280 kutoka Nyakanazi hadi Kigoma.

Kwa mujibu wa Afisa Nishati Mkuu kutoka Wizara ya Nishati, Mhandisi Salum Inegeja, miradi yote hiyo inafadhiliwa na AfDB kwa namna mbili ambazo ni ama kwa ufadhili wa asilimia kadhaa kwa kushirikiana na wadau wengine au ufadhili wa asilimia 100.

Kuhusu hatua ambazo Serikali imechukua katika kuhakikisha inaboresha utendaji wa TANESCO; suala ambalo Ujumbe wa AfDB ulitaka kujuzwa; Waziri Kalemani alisema uboreshaji huo unahitaji kupitia hatua kadhaa ambazo tayari Serikali imeshaanza kuzitekeleza.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni pamoja na kupiga marufuku uagizaji kutoka nje ya nchi, vifaa mbalimbali kama vile nguzo, mashine-umba (transfoma), waya na mita za umeme na badala yake vinunuliwe kwa wazalishaji wa ndani ya nchi.

Alieleza hatua nyingine iliyochukuliwa na Serikali kuwa ni kufupisha muda wa kuwaunganishia wateja huduma ya umeme. “Wateja sasa wanaunganishwa ndani ya siku zisizozidi Saba tofauti na awali ambapo zoezi hilo lilikuwa likichukua muda mrefu zaidi.”

Vilevile, Waziri alieleza kuwa Serikali inazungumza na kampuni za ugavi na usambazaji ambazo zinaidai TANESCO madeni makubwa kusamehe tozo za riba kwa shirika hilo ili kulipunguzia mzigo.

Aidha, hatua nyingine iliyochukuliwa ni kuanzisha na kuwafungia wateja wote mfumo wa Mita za umeme za LUKU zinazowezesha kufanyika kwa malipo ya umeme kadri ya matumizi ya mteja husika.

Mawaziri Kalemani na Mpango, waliahidi kuwa Serikali itaweka jitihada za makusudi katika kuhakikisha kwa upande wao wanatekeleza kwa wakati majukumu yote waliyoafikiana ili kuwezesha miradi yote inayohusika inatekelezwa kikamilifu na kwa wakati kama ilivyopangwa kwa manufaa ya wananchi na Taifa kwa ujumla.

Waliwaagiza wataalam katika Wizara zao kukutana na kujadiliana na wataalam kutoka AfDB ili kuweka mambo sawa, kwa ajili ya kuharakisha utekelezaji wa miradi husika.

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (kushoto), akizungumza katika kikao baina ya Serikali na Ujumbe kutoka AfDB (hawapo pichani), kuhusu utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo. Kikao hicho kilifanyika Aprili 11 mwaka huu, Dodoma. Kulia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani.
Ujumbe kutoka AfDB wakiwa katika kikao baina yao na Serikali (hawapo pichani), kujadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo. Kikao hicho kilifanyika Aprili 11 mwaka huu, Dodoma.
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani (wa tatu-kulia), Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango (katikati) na Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB – Sehemu ya Mashariki, Gabriel Negatu (wa nne–kulia), wakiwa katika picha ya pamoja na wataalam wa Serikali pamoja na Ujumbe wa AfDB, baada ya kikao baina ya pande hizo mbili kilichojadili utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayofadhiliwa na Benki hiyo Aprili 11 mwaka huu, Dodoma.

Kutoka kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, Mkurugenzi Mtendaji wa AfDB – Sehemu ya Mashariki, Gabriel Negatu na Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani wakijadiliana jambo baada ya kikao baina yao, Aprili 11 mwaka huu, mjini Dodoma.