Na. Zuena Msuya,
Simiyu
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amewaagiza
wakuu wa wilaya kote nchini kuwachukulia hatua za kisheria wakandarasi
watakaoshindwa kuunganisha vijiji kuanzia vitatu (3) na kuendelea wakati
wakitekeleza mradi wa usambazaji wa umeme vijijini Awamu ya Tatu (REA III).
Dkt. Medard Kalemani aliyasema hayo wakati wa ziara
yake ya kikazi ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa mradi wa REA III katika
vijiji vya Gumali na Malampaka vilivyopo wilayani Maswa mkoani Simiyu.
Aliweka wazi kuwa wakandarasi wote waliokwisha anza
utekelezaji wa REA III wanatakiwa kuunganisha vijiji kuanzia vitatu (3) na
kuendelea ili kuwatia hamasa wananchi katika kujiunga na huduma ya umeme.
Alisema zoezi hilo litaongeza chachu kwa wananchi
kuanzisha viwanda vidogo vidogo na hata vikubwa mapema zaidi ili kuunga mkono
azma ya Serikali ya Awamu ya Tano katika kutimiza sera yake ya kuwa na viwanda nchini
kote.
"Kila mkandarasi aliyekwishaanza kazi ya
kutekeleza Mradi wa REA III, anatakiwa kuunganisha huduma ya umeme katika
vijiji 3 na kuendelea ndani ya wiki moja, haya ni makubaliano, atakayeshindwa
kufanya hivyo, Mkuu wa Wilaya husika atamkamata na kumtia ndani ",
alisistiza Dkt. Kalemani.
Vilevile aliwaagiza Wakuu hao wa wilaya kwa kushirikiana na Mameneja wa Shirika la
Umeme Tanzania (TANESCO) kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mradi wa REA III
katika maeneo yao ili kuweza kufikia lengo lililokusudiwa la kuunganisha vijiji
vyote na vitongoji vyake ifikapo mwaka 2021.
Aliwasisitiza wakandarasi kuwa ili kurahisisha
utendaji kazi wao na kupunguza gharama watumie
nguvu kazi kutoka katika maeneo yanayozunguka mradi husika ili wananchi wa maeneo hayo
waweze kunufaika na mradi huo kwa namna moja au nyingine na si kuchukua
wafanyakazi kutoka mbali na eneo la mradi.
Akizungumzia hali ya upatikanaji wa umeme katika
mkoa wa Simiyu, Dkt. Kalemani alisema ifikapo mwezi Mei mwaka huu wataanza
kujenga vituo viwili vya kupokea na kupoza umeme ili kupunguza adha ya kukatika
mara kwa mara kwa huduma ya umeme katika mkoa huo. Adha ya kukatika kwa umeme
unatokana na umeme kusafirishwa umbali mrefu kutoka Mkoa wa Mwanza na Mara.
Kwa upande wake, Mbunge wa Maswa Magharibi, Mashimba Ndaki aliwasihi wananchi katika
vijiji vyote vinavyopitiwa na mradi wa REA III
kuchangamkia fursa ya kuunganishwa na huduma ya umeme wa REA III kwa kuwa
ni wa bei nafuu ya shilingi elfu Ishirini na Saba tu (27,000).
Hata hivyo aliwataka wale wote ambao bado hawajafanya
wiring katika nyumba zao kufanya
hivyo haraka. Aidha, kwa wale wenye nyumba za nyasi wawe tayari kutumia kifaa
kinachoitwa Umeme Tayari (UMETA) wakati wa utekelezaji wa mradi huo.
Pia amewaomba wakandarasi wanaotekeleza miradi ya
REA III kushirikiana na Serikali za vijiji na Mitaa wanapokuwa wakihitaji nguvu
kazi ya vijana ili waweze kupata vijana waaminifu na wenye kufanya kazi kwa
uzalendo.
Waziri wa Nishati Dkt. Kalemani (katikati)
akizungumza na wakazi wa kijiji cha Gumali, wilayani Maswa alipofika kukagua
mradi wa REA III.
|
Kikundi cha ngoma ya asili kikitumbuiza kufurahia
huduma ya umeme kufika katika kijiji cha Gumali wilayani Maswa, mkoani Simiyu.
|