Na Zuena Msuya, Kahama Shinyanga.
Waziri wa Ardhi, Nyumba na
Maendeleo ya Makazi Wiliam Lukuvi amewapiga marufuku wananchi wenye tabia ya
kuvamia maeneo yanayopitiwa na miradi mikubwa ya maendeleo kwa Lengo la kulipwa
fidia ikiwemo Mradi wa ujenzi wa Bomba la kusafirisha mafuta ghafi kutoka Hoima
nchini Uganda hadi Bandari ya Tanga nchini Tanzania.
Lukuvi aliyasema hayo wakati
akizungumza katika Warsha ya Wadau wa Bomba la kusafirisha Mafuta ghafi kutoka
Hoima nchini Uganda Hadi katika bandari ya Tanga nchini uliofanyika wilayani
Kahama,mkoani Shinyanga kwa Lengo la kutoa elimu juu ya mradi wa Bomba Hilo.
Alifafanua kuwa baadhi ya
wananchi wamekuwa na tabia ya kuvamia maeneo yanayopitiwa na miradi mikubwa na
kuyaendeleza kwa kupanda miti na kujenga nyumba ili waweze kulipwa fidia, Jambo
ambalo halikubaliki.
Aliweka wazi kuwa mpaka sasa
tayari wameshapiga Picha za awali katika maeneo yote yatakayopitiwa na mradi
huo ili kurahisisha zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi watakaoposha mradi huo.
“Kuna baadhi ya wananchi wakiona
mradi mkubwa unapita wanaanza kuweka nguvu kubwa ya kujenga nyumba ambazo
haziishi watu ili mradi tu wategeshe, mwingine anahamisha miti ya minazi au
mkorosho ili afidiwe, hii si sawa! wananchi acheni tabia hiyo, na kila mmoja
awe mlinzi kwa mwenzake na tuelezane ukweli kuhusu Miradi ya Maendeleo kwa
faida yetu sote," Alisema Lukuvi
Akizungumzia zoezi la ulipaji
fidia, Lukuvi alisema Serikali haitamuonea mtu yeyote na kila mmoja atalipwa
kile anachostahili kulipwa kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi.
Aidha aliwataka Maafisa Ardhi kwa
kushirikiana na Viongozi wa Serikali za Mitaa pamoja na vijiji kutoa elimu
sahihi juu ya ulipaji wa fidia kwa wananchi kwa mujibu wa Sheria ya ardhi ili
kuepusha changamoto zitakazoweka kujitokeza hapo baadaye.
Lukuvi aliweka wazi kuwa katika
zoezi la ulipaji wa fidia kwa wananchi viwango vitakavyotumika ni vile
vilivyopo katika Sheria ya Ardhi ya Tanzania hivyo wananchi waridhike na kile
watakacholipwa kwa wakati huo.
Aidha aliwataka wananchi kutokwamisha
ujenzi wa mradi huo kwa namna moja ama nyingine pia amewasihi kushirikiana na
wale watakaokuwa wakifanya kazi katika maeno husika ili kurahisisha
ukamilishwaji wa ujenzi wa Bomba hilo kwa haraka zaidi kwa kuwa mradi huo una
manufaa kwao na taifa kwa ujumla.
"Endapo mtu amejenga eneo la
hifadhi ambapo Bomba hilo litapita hatalipwa fidia, kwa kuwa fidia itatolewa
kwa wale tu ambao maeneo ya yemepitiwa na Bomba hilo na si wale waliovamia
maeneo ya hifadhi ya barabara kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi," alifafanua Lukuvi.
Mradi wa Ujenzi wa Bomba la
kusafirisha mafuta ghafi unahusisha Wizara na Taasisi mbalimbali za Serikali ili
kufanikisha ujenzi wake ikiwemo Wizara ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara
ya Maji na Umwagiliaji, Wizara ya Fedha na Uchumi, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano pamoja na Wizara ya Mambo Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.